NIMEWAHI
kuzungumza mara kadhaa katika safu hii kuhusu huyu binti, mtoto wa
nguli wa zamani wa soka Tanzania, Ezekiel Greyson ‘Jujuman’, aliyevuma
sana akiwa na Simba. Anaitwa Aunt Ezekiel, staa wa filamu za Kibongo!
Nilisema kuwa katika tasnia ya filamu, ni muigizaji mzuri kwa kupamba
sinema kutokana na uzuri wa sura na umbo lake, lakini katika wasanii
wanaotakiwa kwa weledi na viwango, bado ni mtu wa kati, ingawa akiwa
makini zaidi katika kazi yake, anaweza kuja juu!
Aunt, kama walivyo wasanii wenzake wenye majina, anavuma zaidi nje ya
fani kuliko ndani. Wakati waigizaji kama Natasha, Aisha, Monalisa na
Nora enzi zao walivuma kutokana na uwezo wao katika kazi wakiwa na
makundi yao runingani, kizazi cha kina Aunt Ezekiel kinatikisa anga
kikiwa katika kumbi za starehe na kwenye mikusanyiko ya watu!
Leo nazungumza tena na Aunt, hasa baada ya kujiuliza kwa muda mrefu
na kushindwa kupata jibu, la kama muigizaji huyu yupo katika ndoa au
alishaachika tena. Kumbukumbu zinaniambia aliwahi kuishi kwa kupika na
kupakua na mtoto mmoja wa mjini, Jack Pemba na baadaye Hartman Mbilinyi
kabla ya ndoa yake ya mwisho akiwa na Sunday Demonte.
Ingawa ni vigumu kuthibitisha, lakini ushahidi wa mazingira
unaonyesha Aunt Ezekiel ni mmoja wa waigizaji wa kike ambao hawajatulia.
Msanii huyu anadai yupo katika ndoa na mumewe Demonte, ambaye anaelea
katika uvumi kwamba huko aliko, yupo matatizoni.
Ni kipindi kirefu tokea mumewe alipoondoka nchini kuelekea Ughaibuni.
Sipendi sana kumuongelea yeye kwa sababu hayo ni masuala ya kibinafsi,
lakini hili la Aunt linanipa ugumu kidogo kulikalia kimya.
Aunt anadaiwa kutoka kimapenzi na bwana mdogo mmoja mcheza shoo wa
Diamond, anayeitwa Moses Iyobo. Mapenzi yao yalianza kwa siri, lakini
wenyewe mara kadhaa kwa nyakati flani wamewahi kunukuliwa wakisema kuwa
hawaachani ng’o!Iyobo anadaiwa pia kuwa na mke, ambaye aliwahi hata
kuleta kasheshe kubwa baada ya kubaini uhusiano huo.
Ninajiuliza, Aunt ameolewa, shemeji na wifi zake wapo hapahapa mjini,
inakuwaje anafanya mambo hadharani namna hii?Anyway, huenda basi hayo
ni mambo ya familia, wanajuana wenyewe, lakini kwa jamii inayomtazama
huyu binti, hasa watoto, anaifundisha nini kuhusu maisha ya ndoa?
Kwamba unaweza kumuacha mumeo Mwanza, ukaja Dar es Salaam na kutanua
tu ovyo na waume wa wenzio? Huenda, kama ni kweli kwamba mumewe yupo
matatizoni, kama binadamu anaweza kujikuta akiwa na mahitaji ya
kimaumbile.
Kama ni hivyo, sasa kuna tatizo gani kufanya kwa siri? Watu kibao tu
wanafanya michepuko nje ya ndoa, lakini si wanafanya kwa kujificha ili
kulinda heshima ya familia zao?
Lipo tatizo la msingi ambalo linapaswa kurekebishwa na huyu dada
haraka. Kama ametengana na mumewe, aweke hadharani ili kupunguza maswali
haya, kwa vile mashabiki wake na wale wa fani yake kwa jumla, wajifunze
nini kwake, kwamba unaweza kuolewa au kuoa na wakati huo huo ukawa huna
hofu na penzi lingine?
Hapana, huu ni uhuni usiokubalika. Kuoa au kuolewa kunamaanisha ni
mwisho wa maisha yako ya kutangatanga kingono, umeamua kutulia kwa mmoja
umpendaye. Kama alikuwa bado hajatosheka kwa nini alijiongopea?
Jambo lingine la kumshauri ni kuwa umri unasogea, asije kujikuta
anazeeka na ujana bado haujamwisha, kwa sababu kwa jinsi anavyoyaendesha
maisha yake, ni kama vile nayo anaigiza kama anavyofanya kwenye filamu!