Katika hali ya kushangaza, mtu mmoja anayefahamika kwa jina la
Ali, mkazi wa Mwananyamala jijini Dar, amekamatwa na polisi baada ya
kudaiwa kuunganisha visivyo halali, mitambo ambayo iliwawezesha watu
kuangalia matangazo ya televisheni ya vituo mbalimbali kwa malipo
rahisi.
Bw.
Ali anayedaiwa kuunganisha visivyo halali, mitambo ya kurusha matangazo
ya televisheni ya vituo mbalimbali kwa malipo rahisi.
Awali,
msamaria mwema mmoja alipiga simu kwa kikosi kazi cha Operesheni Fichua
Maovu (OFM) cha Global Publishers na kukitonya juu ya uwezo wa mtu huyo
anayewashangaza kwa utaalamu wake wa kuunganisha mitambo hiyo bila
kugundulika.“Hapa kuna watu kama 80 hivi wameunganishwa, wanaangalia televisheni za Azam, Zuku na nyingine kwa bei chee, lakini wanaangalia mipira, filamu na kila kitu, yaani huwezi kuamini kaka,” chanzo hicho kilinyetisha kwa OFM.
Katika kujiridhisha, kikosi kazi chini ya kamanda mkuu, kilitembelea eneo la tukio na kufanya ukaguzi wa siri, uliothibitisha kuwepo kwa huduma hiyo, lakini bila ya kuwepo kwa dekoda za vituo hivyo vya televisheni vinavyotolewa kwa malipo.
Baada ya kujiridhisha huko, OFM ilifanya mawasiliano na wahusika wa vituo hivyo, ambao nao walitembelea eneo hilo la tukio na kujionea wenyewe. Wahusika hao walikuwa ni Afisa Leseni wa DSTV na Afisa Mauzo wa Azam Tv pamoja na mtu mmoja kutoka chama cha hakimiliki cha COSOTA.
OFM iliwashauri maofisa hao kuripoti jambo hilo kituo cha polisi, ushauri ambao waliukubali na kwenda kutoa taarifa Kituo cha Polisi Oystebay ambao waliongozana na watu hao hadi Mwananyamala.
Madishi ya Satelaiti yanayotumiwa na Bw. Ali kurushia matangazo ya televishen yakiwa juu ya nyumba yake.
Kufika nyumbani kwa mtuhumiwa huyo ambaye pia ni maarufu kwa jina la
utani kama Masetelaiti, Polisi walifanikiwa kumkamata na baada ya
upekuzi, waligundua kuwepo kwa mitambo ya aina mbalimbali, vikiwemo
ving’amuzi vya aina mbalimbali, modulators, Receivers na vifaa vingine
vikionekana vikiwa vimeunganishwa kwa utaalamu wa hali ya juu katika
ukuta wa sebule yake.Masetelaiti alikiri kuendesha maisha kwa staili hiyo na kudai kuwa utaalamu wa kuunganisha ving’amuzi hivyo ni wake mwenyewe na amekuwa akifanya hivyo kwa muda mrefu.
Afisa Leseni kutoka Cosota, Zephania Lyamuya alisema jamaa huyo anastahili kupelekwa Polisi kutoa maelezo kwani licha ya kutokuwa na leseni ya kufanya biashara hiyo, pia amekuwa akiwanyonya waigizaji wanaostahili kulipwa kila filamu zao zinaporushwa katika televisheni za nje.
Naye Afisa Mkuu wa Mauzo kutoka kampuni ya Azam aliyejitambulisha kwa jina la Shah Seffu (pichani kulia), alisema kuwa operesheni hiyo ni moja kati ya hatua walizozipanga kumaliza tatizo la kuingilia mawasiliano ya televisheni jambo ambalo limeonekana kukua kwa kasi nchini.
Baada ya kuvikusanya vifaa hivyo vilipelekwa katika Kituo cha Polisi cha Oysterbay sambamba na mtuhumiwa kutoa maelezo ambapo jalada lilifunguliwa OB/RB/16106/2014, KUINGILIA MAWASILIANO YA TELEVISHENI