Vidonda
vya tumbo ni ugonjwa unaowasumbua watu wengi, wanaume na wanawake na
hata watoto wadogo. Tatizo hili husumbua sana na kumfanya mgonjwa
asiweze kumudu shughuli zake za kila siku.
Ugonjwa huu huathiri kwa ujumla katika suala zima la afya.
Tatizo hili huanza taratibu na dalili za awali huwa hazionyeshi kama mtu ana ugonjwa huu.
Chanzo cha ugonjwa
Ugonjwa huu hutokana zaidi na
maambukizi ya bakteria waitwao ‘Herictobacter Pylori’ au maarufu kama
H. Pylori hushambulia tabaka la ndani la tumbo.
Aina hii ya bakteria ni wagumu kufa kwa kuwa wana uwezo wa kuishi
kwenye mazingira ya tindikali tumboni. Tumboni kuna tindikali ya
Hydrochloric Acid ambayo husaidia katika mmeng’enyo wa chakula.
Bakteria hawa wanaposhambulia tabaka la ndani la kizazi, hutegemea
vishimo vishimo ambavyo ni vidonda hivyo tindikali inapotoka huchoma
kwenye hivyo vidonda na kumfanya mgonjwa ahisi maumivu makali.
Aina za vidonda vya tumbo
Vidonda vya tumbo vipo vya aina mbili,
kwanza ni vile vilivyopo mwanzoni mwa tumbo la chakula, Gastric Ulcers
na ya pili ni Duodenal Ulcers katika sehemu ya pili ya tumbo. Maumivu na
dalili za aina hizi mbili hufanana sana.
Ili kutofautisha aina hizi za vidonda, vipimo maalum hufanyika kama
vile ‘OGD” na “Barium Meal’, vipimo ambavyo hufanyika katika hospitali
za rufaa.
Dalili za ugonjwa
Hapa tutazungumzia dalili kuu
za vidonda vya tumbo kwa ujumla. Mgonjwa wa vidonda vya tumbo katika
hatua za awali huwa hajigundui kama ana tatizo.
Mgonjwa hulalamika kuhisi homa za mara kwa mara na kujihisi kama ana
malaria au homa ya tumbo ‘Taifoidi’, wengine hulalamika kutumia sana
dawa za taifoidi lakini hakuna nafuu.
Mwili unanyong’onyea, maumivu ya viungo, kuhisi baridi kuumwa kichwa na tumbo kujaa gesi.
Mgonjwa pia hulalamika maumivu ya tumbo eneo la chembe ya moyo ambapo ni chini ya kifua na juu ya kitovu.
Maumivu ya muda mrefu husambaa tumbo lote na tumbo huunguruma mara kwa mara .
Maumivu ya chembe ya moyo yaani chini ya kifua na juu ya kitovu husambaa hadi kifuani na kuzunguka mpaka mgongoni.
Mgonjwa hulalamika kuhisi moto kifuani na maumivu yaani kiungulia.
Akilala usiku hali ya moto huongezeka na mgonjwa akicheua hutoa majimaji
ya moto na machungu.
Mgonjwa hupata choo kigumu na vipande vipande kama cha mbuzi na wakati mwingine huwa cheusi.
Mgonjwa hupoteza hamu ya kula na wakati mwingine hutapika damu. Macho
hupoteza nguvu ya kuona kwa kuwa muda wote anakuwa na maumivu, mwili
unachoka na anakosa raha kutokana na kuwaza sana juu ya maumivu
anayopata kiasi cha kumfanya mgonjwa akonde.
Mkojo unakuwa wa njano sana, hufunga kupata choo kikubwa na
kusababisha maumivu ya kiuno kwa ndani ambayo husambaa hadi miguuni.
Hamu ya tendo la ndoa pia hupotea.
Uchunguzi wa ugonjwa
Uchunguzi wa awali
hufanyika katika vituo vya afya na hospitali za wilaya, mikoa na rufaa.
Ni ugonjwa unaotibika hospitali na vipimo ni kama Ultrasound, OGD,
Barium Meal na vipimo vya damu ili kuangalia maambukizi ya H. Pylori na
wingi wa damu.
Choo kikubwa pia kitapimwa. Ni muhimu pia kuangalia matatizo mengine
kwa undani. Kipimo cha OGD ambacho kitapitishwa katika mfumo wa chakula
kitasaidia kutoa majimaji yatakayopimwa maabara.
Ushauri
Ni vema mgonjwa azingatie kuhudhuria hospitali kwani
ugonjwa wa vidonda vya tumbo huchunguzwa na kutibiwa hospitali ingawa
tiba huchukua muda mrefu.
Ugonjwa huu dalili zake zinafanana sana na saratani au kansa ya tumbo
hivyo ni vizuri uwahi hospitali ili ugundulike mapema.Unaweza ukawa
unatumia dawa nyingine pasipo uchunguzi wa kidaktari mwishowe ukajikuta
tayari hali inakuwa mbaya na kusababisha utumbo kutoboka au kansa.