MKAZI wa Buhare, Manispaa ya Musoma, Patrick Wambura (33) ambaye ni mwalimu wa kujitegemea Shule ya Sekondari Makoye, anashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Mara kwa tuhuma za kuiba mtoto wa kike wa miaka minne.
Mwalimu huyo alifanya wizi huo Novemba 15 mwaka huu maeneo ya Nyasho stendi kwenye mgahawa wa Anastazia Hitra (28) anayedaiwa kuwa mama mzazi wa mtoto huyo.
Akizungumza na waandishi wa habari Anastazia alidai kuibiwa mtoto aliyemtaja kwa jina la Aisha Nelson (4) akiwa naye kwenye mgahawa huo na kueleza kwamba mtuhumiwa alikwenda hapo kupata supu na chapati.
Anastazia alisema wakati akifuatilia malipo yake kwa mteja huyo, ndipo alipogundua mtoto hayupo na kuanza kumtafuta ambapo alifanikiwa kumpata maeneo ya zahanati umbali wa mita 500 kutoka mgahawani hapo akiwa na mtuhumiwa aliyekuwa anajiandaa kupanda pikipiki.
“Nilipomuona akiwa na mwanangu nilipiga yowe kuomba msaada kwa wananchi ambao walinisaidia kumkamata huyo mwizi ila mtoto wangu alikuwa salama,” alisema.
Jeshi la Polisi linaendelea kumshikilia mtuhumiwa na kwamba atafikishwa mahakamani muda wowote baada ya upelelezi kukamilika.