CHADEMA YAIONA CUF NI KIBARAKA WA CCM, SOMA KUJUA UKWELI


BAADHI ya wafuasi cha Chadema, jana nusura waanzishe fujo kwenye mdahalo wa kujadili demokrasia na migogoro ndani ya vyama vya siasa, baada ya mmoja wa washiriki kutamka kuwa, CCM itaendelea kuongoza nchi endapo vyama vya upinzani vitaendelea kuwa na migogoro hivyo kuzidi kividhoofisha.

 
Kauli hiyo, licha ya kutaka kusababisha fujo, iliwafanya baadhi ya wafuasi wa Chadema kutoka nje ya ukumbi.
 
Rehema Mwenda wa Chama cha Wananchi (CUF), ndiye aliyepasua ukweli huo uliowakera baadhi ya wafuasi wa vyama vya upinzani, baada ya kusisitiza migogoro katika vyama haina faida zaidi ya kuvidhoofisha, huku CCM ikizidi kujipanga na kuonya kuwa, migogoro ikiendekezwa ni sawa na kuipa CCM fursa ya kuendelea kuongoza nchi.
 
Katika mdahalo huo ulifanyika jijini Mwanza  ilizuka sintofahamu wakati mtoa mada ya “Hali ya Siasa - Tulikotoka, Tulipo na Tuendako”, Habibu Change alipokuwa akiwasilisha mada yake na kudai kuwa ndani ya Chadema kuna mgogoro, kauli iliyopingwa na Wana-Chadema na wengine kutoka nje kabisa ya ukumbi wa mjadala.
 
Akichangia katika mdahalo huo, Shaban Ironga alisema migogoro ndani ya vyama vya siasa imekuwa ikidumaza demokrasia ya kweli na mawazo ya kweli kutokana na maamuzi ya wachache na faida ya wachache.
 
“Demokrasia ya kweli hujengwa na wanachama kuanzia ngazi ya chini na kwamba wapo waliogombana na kupoteza ndugu zao kutokana na vyama hivi lakini leo wanaonekana sio watu ndani ya vyama kutokana na ubinafsi na maamuzi ya wachache,” alisema.
 
Aidha Ironga aliwataka wanachama wa vyama vya siasa vya upinzani kuamka na kuacha kutumika na viongozi kwa ajili ya maslahi yao kwani wamekuwa wakipoteza nguvu zao huku wanzao wakiendelea kunufaika.
 
Awali akitoa mada ya kwanza ya demokrasia na migogoro ndani ya vyama vya siasa, Jimmy Luhende alisema hakuna siasa ya kupendana kwenye mapambano na kwamba wakitokea marafiki ujue wanaanza kupotosha jitihada za mapambano.
 
Mdahalo uliokuwa ukijadili migogoro ndani ya vyama vya siasa inakuza demokraia au la, uliandaliwa na Asasi ya Jitambue Foundation ambapo walilazimika kuita mabaunsa ili kudhibiti vurugu zilizotaka kujitokeza.

-Habari Leo