PATA KUFAHAMU SIRI YA MAPACHA WA KIKE NA WAKIUME WA SNURA.


Kila anapopanda jukwaani huambatana na ‘pacha’ wake wanaopamba maonyesho yako, kuongeza ladha ya muzikin wake. Huyu siyo mwingine bali ni msanii wa muziki wa mduara, Snura Mushi
anayetamba na wimbo Nimevurugwa, baada ya wimbo wa Majanga aliourekodi mwishoni mwa jana. Snura anamiliki madansa wanne ambao ni Farida na Faidha Jafari, hawa wasichana. Lakini pia anao wacheza shoo wa kiume; Elisha na Eliya Askofu.

Siyo rahisi kuwatofautisha madansa hao mahiri kutokana na kufanana,pia kuonyesha kuipenda kazi yao na kuithamini wakiwa na viwango sawa vya uchezaji.
Baadhi ya mashabiki waliowahi kuhudhuria maonyesho Snura, bila shaka hupata wakati mgumu kuwatofautisha madansa hao kwa kuwa mfanano wao ni kuanzia miili, uchezaji hadi nguvu wanazozitumia kwa pamoja wawapo jukwaani.
Starehe lilimtafuta Snura ili kujua kwa undani kuhusu uamuzi wake wa kufanya kazi na pacha hao na alipowapata, ambapo alianza kwa kueleza kuwa binafsi alitumia zaidi ya mwezi mmoja kuweza kuwatofautisha.
Mwandishi: Madansa wako mbona wanafanana sana kiasi cha kushindwa kuwatofautisha?
Snura: Nina madansa wanne. Hawa ni pacha wa mfuko mmoja,wasichana walizaliwa katika familia ya Mzee Jafari, wavulana wanatoka katika familia ya Askofu.
Mwandishi: Kwa nini uliamua kuchukua pacha na kuwaajiri kama madansa wako?
Snura: Ilitokea tu. Awali, nilikuwa na madansa lakini waliondoka na nikabaki na mmoja. Nikaamua kutafuta mwingine mmoja wa kike na bahati nzuri nilipata wawili ambao ni pacha. Niliamua kuwachukua wote, hata hivyo yule mmoja hakudumu akaondoka nikabaki na hawa wawili ambao ni pacha. Siku isiyo na jina meneja wangu alinipigia simu na kuniambia kuwa amepata pacha wengine hivyo niongeze idadi ya dansa. Nilikubali na mara nilipokutana nao nilistaajabu kuona nao wamefanana sana.
Mwandishi: Unawezaje kuwatofautisha?
Snura: Mwanzoni ilikuwa ngumu ilinichukua muda mrefu kuwajua na kutofautisha. Ilifikia hatua nikimwita Farida nahisi amekuja Faidha,vivyo hivyo kwa hawa wavulana, lakini sasa kuna alama ambazo zinanitambulisha, naweza kuwatofautisha. Ila wenyewe wanapenda kusuka sare hata wale wa kiume nao wananyoa kiduku wote wawili ni ngumu kwa aliye mbali nao kuwatofautisha.
Mwandishi: Imewahi kutokea pacha hawa wakagombana, huwa unachukua hatua gani katika kuwasuluhisha?
Snura: Mapacha wanajulikana tabia zao. Kugombana wanagombana, tena inaweza kutokea wakaanzisha ugomvi muda mbaya, unaona tunakwenda kufanya shoo wanaanza kugombana hadi tunaingia kwenye gari, ila mimi huwawafokea kwa kuwa sipendi wagombane.