KAMA
mwandishi, sijawahi kukutana na Kajala Masanja na kufanya mazungumzo
naye, lakini kama mdau nimeona kazi kadhaa za muigizaji huyu mwenye jina
kubwa katika Bongo Movie.Anajitahidi kuigiza na katika uhalisia wake,
huyu ni miongoni mwa wadada wanaoweza kuibeba tasnia hii na kuifikisha
katika levo zingine za mbali na kuiletea sifa nchi yetu.
Nimewahi kusoma simulizi juu ya maisha yake, inasisimua sana, hasa
alipokuwa akizungumzia sakata lililosababisha yeye na mumewe kukamatwa,
kufikishwa mahakamani na hatimaye kuhukumiwa jela. Amepitia maisha
yanayotosha kumpa mifano na mafunzo mengi ya maisha.
Kama siyo shoga yake Wema Sepetu kumlipia fedha za faini
alipohukumiwa pale Kisutu mwaka mmoja uliopita, hivi sasa tungekuwa
angalau tumeanza kumsahau Kajala, kama ilivyo kwa mume wake Agostino
Faraji.
Lakini unapomuona maisha anayoishi hivi sasa, unashindwa kujizuia
kujiuliza kama ana chochote cha kujifunza na kujutia katika maisha
anayopitia, hasa katika matumizi ya fedha.Wanaomfahamu vizuri wanasema
hivi sasa msichana huyu ana fedha za kutosha, kiasi cha kumfanya atembee
akiwa na wapambe, si unajua tena kibongobongo?
Sijajua ni fedha kiasi gani, lakini unapomuona msichana kama Kajala,
anakwenda kumtunza mtu burungutu la shilingi laki sita na ushee, ni
lazima ukubali kuwa anazo za kutosha.
Enzi za ujana wetu, tulizoea kuwaona watu walioitwa Mapedeshee
wakifanya madoido hayo katika kumbi za starehe na kwenye mikusanyiko. Na
ninawakumbuka bado, akina Fikiri Madinda, Juma Banatoz ‘JB’, Papaa
Msofe, Muzamil Katunzi, Papaa Chosta, Hussein Makabyureta, Rama Mutoto
ya Ng’ombe, Jack Pemba ‘JP’ na wengineo wengi wa enzi zao.
Sitaki sana kuingia kwa undani kujua nini kimewasibu watu hawa kwa
sasa, lakini ushahidi wa mazingira unaonyesha jamaa wamebadili staili ya
maisha, bila shaka baada ya kugundua walikuwa wanapotea, kwa sababu
walikuwa wanayanunua majina yao kwa bei kubwa sana.
Shoga yake Kajala, Wema Sepetu, miezi michache iliyopita naye alikuwa
katika hali kama hiyo, akitapanya fedha kwa staili ya kutembea na
wapambe wengi, huku akigharamia matumizi yao, hata yale yasiyo na
msingi.
Simfundishi namna ya kutumia fedha zake, lakini ni ushauri tu ambao
anaweza kuufuata au kuushiti. Pesa haitoshi. Anaweza kuziona nyingi leo,
lakini sidhani kama zinaweza kufika kesho.
Katika kutengeneza maisha, kesho iko mbali sana, lakini kwenye matumizi, kesho ni kufumba na kufumbua tu.
Watu wenye fedha zao tunaowajua, hawana ujuha wa kumwaga hela ovyo
kwa lengo la kujitangaza, badala yake kama kurudisha sehemu ya hela kwa
jamii, hula na watoto yatima, wazee wasiojiweza na wakati mwingine
kuwapa mahitaji muhimu kama vyakula na mavazi.
Kajala bado ni binti mdogo. Kuwa na shilingi milioni 50, 100 au
bilioni moja siyo kufika, bali ni mwanzo mzuri wa kutengeneza maisha ya
baadaye. Nimshauri awekeze katika kilimo, majengo au ufugaji, uwekezaji
ambao baada ya miaka michache, fedha zitaanza kutiririka bila kikomo na
hivyo kumpa uhakika angalau.
Hana sababu ya kujenga jina kwa sababu tayari analo ila ana ulazima
wa kujenga maisha kwa vile hana. Sifa za kijinga ndiyo zinazowasumbua
sana wasanii, wanashindwa kuyajenga maisha yao kwa pesa wanazozipata
kutokana na fursa mbalimbali wanazokutana nazo.
Hela zinapokuja hazipigi hodi na uzuri wake zinapoondoka, mwenye
kuzimiliki anajua kuwa zinaondoka. Kajala anamjua Bill Gates? Ni tajiri
wa kutupwa, lakini kila siku anakuwa mtu wa kwanza kufika ofisini kwake,
kuhakikisha utajiri wake hauyumbi.
Leo mdogo wangu Kajala umepata mkondo unautumia kutafuta sifa, badala ya kujijengea misingi imara ya maisha yako ya baadaye!






