HAKUNA lugha nyingine ya
kusema zaidi ya kuainisha kuwa pepo wa ajali za barabarani zinazoua
mamia ya watu ni uzembe wa kutisha unaofanywa na madereva katika
uendeshaji magari bila utii wa sheria. Basi la Mtei Express likiovateki wakati kuna magari mawili yanakuja kwa mbele.
Uchunguzi wa Gazeti la Ijumaa uliofanywa hivi karibuni katika maeneo
mbalimbali nchini umebaini kuwa, mbali na mwendo kasi unaotajwa mara kwa
mara kuwa unachangia ajali, suala la kutozingatia sheria za usalama
barabarani ni hatari zaidi.
Picha za magari ya abiria yaendayo mikoani zilizotumika ukurasa wa
nyuma wa gazeti hili ni kielelezo tosha kuwa madereva wengi hawajui
sheria za usalama barabarani au wanazivunja makusudi jambo ambalo
husababisha kutokea kwa ajali nyingi za magari kugongana uso kwa uso.
Uamuzi wa kizembe kama huo na ule unaonekana katika picha zilizobeba habari hii ambapo madereva wa magari husika wanaonekana ‘kuovateki’ kinyume cha muongozo wa uendeshaji.Sheria zinamkataza dereva kulipita gari jingine kwenye mlima, mteremko mkali na mahali penye kona, lakini kwa mshangao madereva wengi wamekuwa hawazingatii hilo.
“Ukisafiri hasa kwenye barabara kubwa kuna alama zinazokuongoza, lazima dereva uzifuate, lakini madereva wetu hawafanyi hivyo, inawezekana hawajui sheria au wanapuuza kwa sababu adhabu zetu ni nyepesi tofauti na nchi nyingine kama Rwanda,” alisema Mohammed Mpinga, Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini katika mahojiano na gazeti hili hivi karibuni.
Mbali na ulevi baadhi ya madereva wa mabasi yaendayo mkoani wamekuwa wakiendesha kwa mashindano ya kuwahi kufika waendeko ili wasifiwe na abiria kuwa wamewawahisha jambo ambalo mwishowe kuwahi huko huwatokea puani na kuwasababishia ajali.Taarifa ya polisi inaonesha kwamba kwa mwaka jana pekee kulikuwa na ajali 23,842, kati ya hizo ni za mabasi 931, zilizoua watu 313.






